Mchakato wa kusaka makamishna wapya wa IEBC waanza

Jopo la wanachama tisa watakaoendesha uteuzi wa makamishna hao liliapishwa leo Jumatatu katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Martin Mwanje
1 Min Read

Mcahakato wa kuteua makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) unatarajiwa kuanza kwa kishindo baada ya Rais William Ruto kuteua jopo la wanachama tisa kuendesha mchakato huo. 

Jopo hilo liliapishwa leo Jumatatu katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome katika majengo ya Mahakama ya Juu.

Wanachama wa jopo hilo ni pamoja na Kiome Lindah Gakii, Prof. Adams Oloo, James Evans Misati, Nicodemus Kipchirchir Bore na Koki Muli Grignon.

Wengine ni Carolene Kituku, Tanui Andrew Kipkoech, Dkt. Nelson Makanda na Fatuma Saman.

Jaji Koome amelitaka jopo kuendesha shughuli ya uteuzi kwa uadilifu bila kuegemea upande wowote akisema uthabiti wa nchi hutegemea namna mchakato wa uchaguzi unavyoendeshwa.

“Kuaminika kwa chaguzi kunabaini uthabiti na mustakabali wa taifa letu. Historia imeonyesha kuwa chaguzi zinapokuwa huru, za haki na wazi, taifa letu hunawiri,” alisema Koome.

“Jopo la uteuzi lina jukumu kubwa la kuteua wanaume na wanawake wenye maadili ya juu na wanaoaminiwa kuiongoza IEBC.”

Jaji Mkuu ametoa wito kwa taasisi na wadau wote watakaoshiriki mchakato wa uteuzi ikiwa ni pamoja na bunge, wadau wa kisiasa, mashirika ya kijamii, na umma kuhakikisha uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC unafanywa haraka, kwa uadilifu na kwa uwazi.

 

 

Website |  + posts
Share This Article