Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemhukumu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu kifungo cha miaka minne gerezani baada ya kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi.
Uamuzi huo umetolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, na kuhitimisha kesi iliyodumu kwa takribani miezi 19 tangu kukamatwa kwake.
Lissu awali alishtakiwa kwa kosa la uhaini. Hata hivyo hii leo, hakukutwa na hatia ya kosa hilo kupitia kesi ya uhaini namba 000019605 ya mwaka 2025.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa CHADEMA uliokuwa sehemu ya kampeni ya chama hicho ya No Reforms, No Election. Siku iliyofuata, Aprili 10, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na kusomewa mashtaka ya uhaini.
Mashtaka hayo yalihusiana na matamshi aliyodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, katika mkutano na wagombea wa CHADEMA katika ofisi za chama hicho Mikocheni, Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka ulimtuhumu Lissu kwa kutoa matamshi na kuchapisha taarifa zilizolenga kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwa nia ya kutishia Serikali. Lissu alikana mashtaka hayo.
Kesi hiyo ilianza rasmi kusikilizwa Mahakama Kuu Septemba 8, 2025, mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Katika kipindi cha usikilizwaji, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa. Kwa upande wa utetezi, Lissu aliwasilisha mashahidi watano. Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa mahakamani ni matamshi yaliyodaiwa kutolewa na Lissu, ushahidi wa video ya mkutano huo ambayo haikuwasilishwa mahakamani, namna video ilivyosambazwa na tafsiri ya kisheria ya kosa la uhaini.
Taarifa ya BBC