Kenya yajiunga na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake

Tom Mathinji and Radio Taifa
2 Min Read
Kenya yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Kenya inapoungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake , Rais Willian Ruto amesema serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa wanawake na wasichana.

Kiongozi wa alisisitiza kujitolea kwa serikali, kuhakikisha wasichana na wanawake wanapokea misaada wanayoihitaji ili wafanikiwe.

Kupitia ukurasa wa X, Rais Ruto alisema,” Juhudi za serikali ni zaidi ya kushughulikia ukosefu wa usawa na haki, ikinuia kuboresha ustawi wa wanawake humu nchini,”.

Rais alielezea mwelekeo wa utawala wake katika kupanua fursa kwa wanawake na kubuni mazingira yanayoweza kufanikiwa.

Alipongeza jukumu muhimu la wanawake katika uongozi, biashara na uvumbuzi, akisisitiza michango yao katika ustawi wa nchi hii na kutoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono uwezeshaji wa wanawake na kuhakikisha kila mwanamke na msichana wanaweza kuafikia uwezo wao kamili.

Kwa upande wake, waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ametoa wito wa kuharakishwa kwa juhudi za kuunga mkono agenda ya wanawake humu nchini.

Kulingana na Mudavadi wakati ni sasa kwa jamii kutambua juhudi muhimu ambazo wanawake wanahusika katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ya kijamii.

Kupitia ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya wanawake duniani, Mudavadi amesema siku ya wanawake mwaka huu inatoa fursa ya kuimarisha kwa pamoja na kutekeleza ahadi zinazoweza kutimizwa na zenye matokeo chanya yanayoimarisha ajenda ya wanawake kote duniani.

Aidha, Mudavadi alisema uhusiano mkubwa kati ya jinsia, amani na usalama ni nguzo muhimu kwa jamii yenye usawa, isiyobagua na inayozingatia haki ambapo wanawake wamekuwa wahusika wakuu katika uafikiaji wa malengo yaliyodhamiriwa.

Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani mwaka huu “For ALL Women and Girls: Rights, Equality Empowerment” inatoa wito wa juhudi zinazoweza kufumbua nguzo za usawa, haki, uongozi na fursa kwa wote, pamoja na kuweka mustakabali wa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma, na kwamba wote wanahudumiwa kwa usawa.

Siku ya wanawake duniani ni sikukuu inayoadhimishwa kila mwaka kuwa kigezo muhimu cha harakati za haki za wanawake.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article