Vijana milioni moja hapa nchini kupata ajira kupitia mtandao

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa dijitali Eliud Owalo.

Kenya inanuia kubuni nafasi milioni moja za ajira kwa vijana kupitia jukwaa la mtandao.

Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa dijitali Eliud Owalo, alisema hatua hiyo itawapa wakenya ujuzi wa kidijitali na kuwafanya kuwa wajasiriamali badala ya kuwa wanaotafuta ajira.

Akizungumza katika eneo la Kutus kaunti ya Kirinyaga alipokuwa akiongoza maadhimisho ya siku ya kimataifa ya upatikanaji habari, waziri Owalo alisema vijana wanaofuzu kutoka vyuo na vyuo vikuu, hawapaswi kuwa wakitafuta ajira, ila wanahitajika kuwa na ujuzi wa kujiajiri.

Waziri huyo alisema atafika katika bunge la kitaifa kupigia debe kuimarishwa kwa sera za ulinzi wa data kwa wakenya.

Kulingana na waziri huyo, zoezi linaloendelea la kuweka vituo vya kidijitali katika kila wadi, linalenga kuhakikisha kila kijana katika maeneo ya mashinani anapata ujuzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, katibu katika idara ya utangazaji na mawasiliano Prof. Edward Kising’ani, alisema kuna umuhimu wa kuwa na intaneti bila malipo, kwa kuwa wananchi wanahitaji habari.

Share This Article