Mwanamuziki Kevin Bahati alimrejelea mke wake Diana Marua kama mama yake, jinsi amekuwa akitaniwa na wengi, huku akimtakia mema kwenye siku yake ya kuzaliwa.
Bahati alichapisha picha kadhaa za Diana za awali huku akiandika, “Mpendwa Diana, ningependa kukufahamisha kwamba umekuwa mwamba wa familia yetu, uti wetu wa mgongo, shingo yetu, pigo la moyo wangu, mwenzangu katika maombi, rafiki wangu wa dhati, mpenzi wangu na hata mama yangu.”
Mwimbaji huyo kisha aliendelea kwa kumwombea Diana mapenzi ya moyo wake kwa Mungu na kwamba nyota yake iendelee kung’aa.
“Mwenyezi Mungu atimize mahitaji yako na akuonyeshe wokovu wake. Siku njema ya kuzaliwa mke wangu.” alimalizia mwimbaji huyo.
Bahati amekuwa akitaniwa na wengi mitandaoni ambao wamekuwa wakimrejelea kama mtoto wa Diana kutokana na ukweli kwamba Diana amemzidi umri.
Wanandoa hao walijipatia umaarufu kutokana na kazi zao za muziki pamoja na uundaji wa maudhui kwenye mitandao, kazi iliyowapa tija zaidi kwani walipatiwa kipindi cha kuangazia familia yao ambacho kiko kwenye jukwaa la Netflix.