Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amependekeza kuandaliwa kwa mazungumzo ya haraka ya amani kati ya mataifa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda huku vita vikiendelea mashariki mwa DRC.
Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Kanze Dena ambaye ni msemaji wake, Uhuru ambaye ni mwezeshaji wa mpango wa Nairobi unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, alizitaka nchi hizo kukumbatia mazungumzo na kusitisha vita.
Kiongozi huyo alisikitika kwamba mkataba ulioafikiwa awali wa kusitisha vita haukuzingatiwa na hivyo kusababisha mazungumzo ya amani na diplomasia yajikokote.
Uhuru alisema pia kwamba inasikitisha kwamba mpango wa Nairobi wa kutafuta amani unaoongozwa na EAC ulipuuzwa hata ingawa ulikuwa na jukumu muhimu la kuangazia mzozo wa DRC.
Taarifa ya Rais huyo mstaafu inajiri wakati ambapo mwenyekiti wa EAC Rais William Ruto na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wameandaa mkutano.
Mkutano huo wa kutatua mzozo wa mashariki ya DRC utaandaliwa nchini Tanzania na utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais Ruto kama mwenyekiti wa EAC na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Viongozi wa nchi za DRC na Rwanda ambao ni Felix Tshisekedi na Paul Kagame, wameripotiwa kuthibitisha kwamba watahudhuria mkutano huo.