Wakazi wa kaunti ya Kilifi wanahimiza kwamba serikali sasa inafaa kutoka kwa hatua ya majadiiano na kuingia katika hatua ya vitendo.
Hayo yalidhihirika siku ya Alhamisi katika kikao cha tano cha mazungumzo baina ya vizazi kilichoandaliwa katika ukumbi wa jamii wa Kibaoni kaunti ya Kilifi.
Margaret Mwachiru ambaye ni mkazi wa Kiifi alisema, “Kusema ukweli, kijana au mama, akiwa hana chochote cha kufanya na kuleta chakula kwa tumbo, atatoka. Hii hasira na uchungu yote, ni kwa sababu hana chochote anaweza kushikilia.”
Mwachiru aliongeza kusema kwamba watu kama hao hujipata wakiiingilia masuala kama matumizi ya dawa za kulevya na hata itikadi kali akisisitiza, “Sasa tutoke katika step ya kuongea, tujiulize tutafanya nini?”
Kwa upande wake, kamanda wa polisi katika kaunti ya Kilifi Reginad Omaria alipongeza vikao hivyo vya majadiliano kati ya vizazi yanayoandaliwa na Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa kwa ushirikiano na shirika la utangazaji nchini, KBC.
“Majadiliano ni hatua nzuri ambayo tumechukua, hatua ya pili ni kusikilizana ndio tujue tofauti zetu na kutafuta suluhu,” alisema Omaria.
Afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini, IEBC katika kaunti ya Kilifi John Mawasit aipendekeza kwamba vijana wajumuishwe katika kila hatua ya maamuzi muhimu ya taifa na wala sio kuachwa tu kuwa wapiga kura.
Mama Tumaini Elisha ambaye ni mzee wa mtaa wa eneo hilo aliomba kwamba wanasiasa wawe pamoja na wawatafutie vijana fursa za ajira ndio wasiwe na muda wa kufikiria kufanya maandamano.
NCIC ilianzisha vikao hivyo kama njia ya kupunguza pengo ambalo limedhihirika kati ya vizazi.
Awamu za kwanza nne za vikao hivyo ziliandaliwa katika kaunti za Marsabit, Nairobi, Kisumu na Busia huku kikao kinachofuata kikitarajiwa kuwa katika kaunti ya Kwale.
