Ni afueni kwa wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya vya umma kote nchini baada ya serikali na Chama cha Matabibu nchini, KUCO kutia saini makubaliano ya kurejea kazini.
Matabibu hao wamekuwa kwenye mgomo uliodumu zaidi ya miezi miwili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, makubaliano hayo kimsingi yanamaanisha kwamba mgomo huo umemalizika.
“Leo, Wizara ya Afya imefanikiwa kujadiliana na kutia saini makubaliano ya kurejea kazini na Chama cha Matabibu nchini, KUCO, na kimsingi kumaliza mgomo unaoendelea,” ilisema taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya baada ya hafla ya utiaji saini makubaliano hayo.
“Makubaliano haya muhimu yanahusisha mishahara iliyoongezwa, masharti yaliyoboresha ya uajiri, bima ya kina ya afya, fursa zilizoongezwa za utoaji mafunzo na hatua zilizoboreshwa za afya na usalama.”
Aidha, makubaliano hayo yanaangazia mashaka yaliyoibuliwa katika sekta ya afya na kuhakikisha uthabiti wa sekta hiyo.
Katika hafla iliyoshuhudiwa na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni na maafisa wa KUCO, Wizara imekipongeza chama hicho kwa ushirikiano wao na dhamira ambayo imesababisha kufikiwa kwa makubaliano hayo.
Siku chache zilizopita, KUCO ilifikia makubaliano sawia na Baraza la Magavana nchini, CoG.