Rais William Ruto ametoa wito kwa Wakenya kujiandikisha kwa Bima mpya ya Afya ya Jamii, SHIF itakayoanza kutekelezwa tarehe mosi mwezi ujao.
Rais Ruto pia ametoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na serikali za kaunti kuwahamasisha Wakenya kujisajili kwenye bima hiyo na kuwaelezea manufaa yake.
“Uzinduzi wa mpango wa upatikanaji wa afya kwa wote unahitaji kuhusika kwa serikali zote ikiwa ni pamoja na kaunti, kuwaelimisha Wakenya kuelewa manufaa ya mpango huu wenye kuleta mabadiliko na jumuishi,” alisema Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo Alhamisi.
“Tunatoa wito kwa kila mmoja kujisajili kupitia *147# au sha.go.ke kabla ya uzinduzi wa mpango huo Oktoba 1, 2024.”
Ruto aliyasema hayo alipokutana na maafisa wa Wizara ya Afya, Magavana na washikadau wengine wakati maandalizi ya kuzinduliwa kwa mpango wa upatikanaji wa afya kwa wote yakiendelea.
Hadi kufikia sasa, Wakenya milioni 1.2 wamejisajili kwa bima ya SHIF itakayochukua mahali pa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, NHIF huku zoezi la usajili likiendelea kote nchini.
Wanachama milioni 9 wa NHIF watahamia SHIF itakayosimamiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA punde baada ya bima hiyo mpya kuanza kutekelezwa.
Wizara ya Usalama wa Kitaifa imetakiwa kusaidia kufanikisha shughuli inayoendelea ya uandikishaji kwenye bima hiyo na kuuelimisha kuhusu faida ya kujiandikisha kwenye bima hiyo.
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa anasema bima hiyo itazinduliwa na kutekelezwa hatua kwa hatua.
“Tunazindua SHA Oktoba 1, 2024. Ni bima itakayozinduliwa hatua kwa hatua, huku mafao ya bima hiyo yakitolewa kulingana na rasilimali zilizopo,” amesema Dkt. Barasa.
“Tutaendelea kuboresha mfumo huo wakati tukisonga mbele.”