Rais Ruto: Kaunti za Kisii na Nyamira kunufaika na masoko mapya

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto katika kaunti ya Nyamira.

Rais William Ruto amesema Kaunti za Kisii na Nyamira zitanufaika na masoko 15 na saba mtawalia, katika juhudi zinazoendelea za kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyabiashara wadogo.

Rais aliyasema hayo alipokuwa katika ziara kwenye Kaunti za Kisii na Nyamira kukagua na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo siku ya Ijumaa.

Masoko yatakayojengwa ni pamoja na Ogembo, Keumbu, Nyamasege, Keroka, Esise, Kahawa, Kemera, Ikonge na Nyamira mjini miongoni mwa mengine.

Hayo ni baadhi ya masoko 400 yatakayojengwa kote nchini ili kuweka mazingira ya kazi ya kuheshimu kwa wafanyabiashara wadogo.

“Yatakapokamilika, masoko haya yatatatua changamoto za uhaba wa ghala, kuimarisha upatikanaji wa soko kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi. Hatimaye hii itapunguza umaskini miongoni mwa Wakenya,” alisema Rais Ruto.

Akizungumza katika soko la Nyamasege eneo la Bomachoge Chache, Kaunti ya Kisii, Rais Ruto alisema utawala wa Kenya Kwanza unatekeleza kile ulichoahidi nchi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Tuliahidi Wakenya kwamba tukichukua uongozi wa nchi hii, tutaanza kutimiza ahadi tulizotoa. Hivyo ndivyo tunafanya sasa,” alisema Rais Ruto.

Dkt Ruto alitangaza kuwa kituo cha polisi cha Ogembo kitahamishwa hadi Tendere ili kutoa nafasi ya upanuzi wa hospitali ya Ogembo.

“Tumekubaliana na viongozi wenu kwamba tuhamishe kituo cha polisi cha Ogembo hadi Tendere ili kufungua njia ya upanuzi wa Hospitali ya Ogembo,” alisema Dkt Ruto.

Huko Nyansiongo, Rais Ruto alikagua ujenzi wa soko la kisasa la Nyansiongo ambalo litahudumia idadi iliyoongezeka ya wafanyabiashara kwenye mpaka wa Sotik-Kisii.

Kiongozi wa Nchi alikariri kuwa utawala wake umekuja na mipango ya makusudi inayolenga kubuni nafasi za kazi kwa mamilioni ya vijana wa Kenya.

Alitaja nyumba za bei nafuu, vitovu vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika ngazi ya wadi, ujenzi wa masoko na uanzishwaji wa maeneo ya viwanja katika kaunti kuwa baadhi ya maeneo yatakayotoa fursa za ajira kwa mamilioni ya wananchi wa kawaida.

Share This Article