Wabunge wataharakisha miswada iliyopendekezwa pamoja na mikakati mingine inayolenga kuleta mageuzi katika sekta ndogo ya kahawa.
Haya yanajiri baada ya naibu Rais Rigathi Gachagua kuandaa mkutano na wabunge wanachama wa kamati ya kilimo, biashara na viwanda, kundi linalohusika na mageuzi katika sekta ya kahawa pamoja na wabunge wanaotoka katika maeneo yanayokuza kahawa, kutafuta mwelekeo kuhusu mageuzi hayo.
Wabunge hao walikubaliana kufanya kazi pamoja kukamilisha mikakati ya kisheria ambayo imesababisha mashauriano ya kina na wakulima na wadau katika sekta hiyo.
Wabunge hao waliidhinisha mageuzi hayo na kuahidi kuharakisha mchakato wa kufanyia marekebisho sheria ya kahawa.
“Mageuzi hayo hayawezi simamishwa. Baada ya mkutano kuhusu kahawa ulioandaliwa Meru mwezi Juni mwaka huu, makundi ya wakiritimba yalianza kusababisha matatizo kuhusu soko la kahawa na utoaji leseni. Wakati mimi na Rais tulipovalia njuga swala hili tulijua haitakuwa safari rahisi,” alisema naibu huyo wa Rais.
Alisema kuwa utawala wa Rais William Ruto, umejitolea kurejesha sekta hiyo ya kumezewa mate kwa wakulima, kwa kuwaondoa walaghai waliokuwa wakifaidika pakubwa.
Kulingana na naibu huyo wa Rais, wakenya milioni tano husaidika kutokana na sekta ndogo ya kahawa na ni muhimu sana katika uchumi wa taifa hili, akiongeza kuwa Rais William Ruto hatalegeza kamba katika kuleta mageuzi katika sekta hiyo.