Rais Ruto azindua ujenzi wa barabara Nakuru

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akiongoza hafla ya uzinduzi wa barabara, Nakuru.

Rais William Ruto amezindua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 12 ya Kinamba-Murinduku katika eneo bunge la Kuresoi North, kaunti ya Nakuru.

Barabara hiyo inatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mazao, ikiwa ni pamoja na vutunguu, nyanya, pareto na mbogaboga na wakati huohuo kuwaletea wakulima mapato kutokana na shughuli zao za kilimo.

Rais Ruto pia ameahidi kwamba mipango ya kujenga barabara kuu ya Nairobi-Mau Summit imepamba moto.

“Ifikapo mwezi ujao, mwezi wa 11, tutaanza rasmi ujenzi wa barabara kutoka Nairobi kupitia Nakuru hadi Mau Summit,” aliahidi kiongozi wa nchi.

“Lakini sasa nimesema sitaki isimamie Mau Summit pekee. Nataka iendelee mpaka Kericho, ifike Kisumu, ifike Eldoret na hata Malaba.”

Nao uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kinamba-Murindiku unakuja wakati ambapo viongozi wa Nakuru wamelalamikia uwepo wa barabara mbovu ambazo zimefanya iwe vigumu kwa wakulima kusafirisha mazao yao hadi sokoni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa kutunza msitu wa Mau leo Jumatatu, Gavana Susan Kihika alitoa wito kwa serikali kuu kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa barabara katika kaunti hiyo aliyosema ni mstari wa mbele katika kufanya shughuli za kilimo nchini.

Hata hivyo, Kihika alisikitikia miundombinu mibaya iliyozagaa eneo hilo hasa barabara ambayo imefanya iwe vigumu kwa wakulima kusafirisha mazao yao hadi sokoni.

Wito sawia ulitolewa na Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui ambaye pia ni Gavana wa zamani wa kaunti hiyo na Seneta Tabitha Karanja.

Rais Ruto akitumia fursa hiyo kuwahakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba serikali yake itafamnya kila iwezalo kuboresha miundombinu kwa manufaa yao.

Website |  + posts
Share This Article