Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni ametoa tahadhari kali dhidi ya ulaji wa nyama ambayo haijakaguliwa na wahudumu wa afya hasa wakati huu ambapo msimu wa sherehe unaanza kubisha hodi.
Ameonya kuwa ulaji wa nyama ya aina hiyo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa.
Muthoni amesema wahudumu wa afya wa serikali kuu na zile za kaunti, wanashirikiana kwa karibu kutekeleza amri ya kuhakikisha nyama yote ambayo inakusudiwa kuuziwa Wakenya, iwe katika vichinjio au katika buchari za mitaani, lazima iwe imekaguliwa ipasavyo na kuwekwa alama ya ubora.
Kadhalika, tahadhari imetolewa kwa wahudumu wa afya ambao wanapokea rushwa na kutozingatia kanuni za afya huku Katibu huyo akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwa macho ili kuhakikisha watu kama hao wanachukuliwa hatua kali.
Wakati huo huo, wazazi wamehimizwa kushirikiana na watoto wao na kuwatafutia shughuli za kufanya ili wasijitose katika hulka mbaya zinazowenza kuwatumbukiza katika lindi la utumizi wa dawa za kulevya.