Mackenzie apatikana na hatia ya kusambaza filamu bila leseni

Tom Mathinji
1 Min Read
Mhubiri wa kanisa la Good News International, Paul Mackenzie.

Mhubiri anayekumbwa na utata wa kanisa la Good News International Paul Mackenzie, amepatikana na hatia ya kumiliki na kusambaza filamu bila leseni kutoka bodi ya kusimamia filamu hapa nchini.

Mackenzie anashtumiwa kwa kurekodi na kutangaza filamu kupitia kituo chake cha runinga cha Times, bila leseni.

Huku akimpata na makosa hayo, hakimu mkuu mkaazi wa Malindi Onalo Olga, alisema hukumu dhidi ya Mackenzie itatolewa tarehe moja mwezi Disemba.

Mackenzie ambaye amekuwa akizuiliwa rumande kwa siku 208 tangu tarehe 15 mwezi Aprili mwaka huu, anashtumiwa kwa kusababisha mauaji ya watu 429, ambao miili yao ilifukuliwa katika shamba la  Shakahola.

Mahakama ilifahamishwa kuwa, mnamo tarehe 11 mwezi Aprili katika kaunti ndogo ya Malindi, kaunti ya Kilifi, Mackenzie pamoja na wengine, walipatikana na video ambazo zilikusudiwa kuwachochea watoto dhidi ya kuenda shuleni.

Kulingana na ushahidi uliotelwa mahakamani, video hizo pia zililenga kuwachochea wakristo dhidi ya madhehebu ya kihindu, waislamu na dini zingine.

Mhubiri huyo angali anazuiliwa na polisi huku uchunguzi ukiendelea kuhusiana na mauaji katika shamba la Shakahola.

Share This Article