Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema kuwa serikali haitakubali taifa hili kuongozwa na mfumo usiozingatia sheria.
Huku akilaani ghasia zilizozuka Jumatano wakati wa maandamano ya Gen Z, Naibu huyo wa Rais alisema serikali itajizatiti kuzuia visa vya uvunjaji sheria, jinsi ilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya Gen Z Jumatano Juni 25,2025.
Akizungumza Alhamisi wakati wa mkutano wa uwezeshaji wa kiuchumi katika eneo bunge la Kibwezi Mashariki, Kithure Kindiki alikashifu vurugu, akisema vitendo vya aibu vya uhalifu vilivyoshuhudiwa, havitavumiliwa tena kuanzia sasa.
“Matukio ya jana ni ya kusikitisha na ambayo yalisababisha maafa, majeruhi na uharibifu wa mali ya umma na ya kibinafsi, yanarudisha nyuma ukuaji wa kiuchumi na kijamii hapa nchini na kamwe hayatavumiliwa,” alisema Kindiki.
Wakati huo huo, Kindiki alikashifu matamshi ya baadhi ya viongozi wa kidini na mabalozi, akisema walichochea vijana kushiriki ghasia.
Prof. Kindiki alithibitisha uchunguzi umeanzishwa ili kuwatia nguvuni waliopanga na kufadhili ghasia hizo.