Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amelaani vikali ghasia zilizozuka wakati wa maandamano ya Gen Z Juni 25,2025, akizitaja hatua za kuipindua serikali ya Rais William Ruto.
“Yale yaliyotokea jana sio maandamano. Hakukuwa na maandamano ya amani, ila ghasia na uhalifu…. ilikuwa hatua ya kupindua serikali kinyume na sheria. Polisi walifanikiwa kuzuia hatua ya kuipindua serikali,” alisema Murkomen.
Kulingana na waziri Murkomen, ghasia zilizoshuhudiwa katika pembe zote za nchi, hazikuhusishwa kwa vyovyote na uhuru wa kujieleza au haki za kikatiba.
“Waliopanga ghasia hizo walikuwa na mpango wa mapema. Walisambaza mpango huo kupitia mitandao ya kijamii. Mpango huo ulikuwa kuteka nyara Ikulu na Bunge la Taifa ishara kwamba wamefanikiwa kuleta mabadiliko fulani,” aliongeza waziri huyo.
Aidha, Murkomen alidokeza kuwa baadhi ya mijengo ya serikali na vituo vya polisi vililengwa na waandamanaji hao.
“Takriban vituo tisa vya polisi vilishambuliwa, tano kati ya hizo zikiteketezwa katika maeneo ya Dagoretti, Molo na Ol Kalau. Magari 88 ya polisi yaliharibiwa,” aliongeza Murkomen.
Waziri huyo aliongeza kuwa nyumba na biashara za baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa serikali, yalilengwa wakati wa ghasia hizo.
Alisema serikali imeanzisha uchunguzi ili kuwakamata waliopanga na kufadhili ghasia hizo.