Serikali yapanga mabadiliko makubwa katika KBC

Haya ni kulingana na waziri wa mawasiliano William Kabogo aliyezuru afisi za KBC na KNA jijini Mombasa.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali inaendeleza mipango ya kufanyia mabadiliko mashirika ya habari ya serikali ya KBC na KNA ili kuyawezesha kuafikia viwango vya kimataifa vya mashirika ya umma ya habari.

Haya ni kulingana na waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali William Kabogo ambaye alizuru afisi za KBC na KNA jijini Mombasa leo.

Kabogo alisema mabadiliko hayo yatalenga miundombinu, uboreshaji wa uendeshaji wa shughuli za mashirika hayo na uboreshaji wa uwezo wa kidijitali.

Waziri alisema kwamba kwa sasa mashirika hayo mawili yana huduma thabiti ya Internet mojawapo ya viwezeshaji vikuu vya usambazaji laini wa habari na utekelezaji wa mipango.

Akizungumza katika afisi za KBC huko Mombasa Kabogo alisema anaendeleza ziara ya maeneo mbali mbali kote nchini kutathmini utayari wa vituo vya mawasiliano vya serikali kwa mfumo dijitali.

“Tunahakikisha kwamba taasisi zote za umma za mawasiliano zimeunganishwa na mtandao wa kasi ya juu na ulio thabiti, tunapoendesha ajenda ya kidijitali ya Kenya,” alisema Waziri Kabogo.

Wakati wa ziara hiyo, Kabogo alikutana na maafisa wakuu wa mashirika hayo mawili katika eneo la Pwani ambao ni Mohamed Hussein wa KNA, Joseph Cheruiyot wa KBC, msimamizi wa kituo cha redio cha Pwani FM Maximillah Walukhu na wengine.

Maafisa hao walimfahamisha kuhusu changamoto zinazowakumba na zile zinazohitaji kushughulikiwa haraka.

Mabadiliko yaliyopangwa yanatarajiwa kuboresha na kuimarisha utangazaji wa sekta ya umma na mawasiliano ya serikali.

,

Website |  + posts
Share This Article