Maafisa wa polisi wa kituo cha polisi cha Oruba kaunti ya Migori wamemkamata mlanguzi wa mihadarati na kupata bangi ya dhamani ya shilingi 13,728,000.
Baada ya kupashwa habari, makachero hao walimtia nguvuni Edwin Okondo Nyagaga mwenye umri wa miaka 32 akiendesha gari aina ya Toyota Kluger lenye nambari za usajili KBS 517N, katika barabara ya Giribe-Masara.
Baada ya kulipekua gari hilo, maafisa hao wa polisi walipata magunia manane ya bangi yenye uzani wa kilo 457.6 yaliyokuwa yamejaa hadi pomoni.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, ilisema maafisa hao pia walipata nambari za usajili wa magari ambazo ni KBP 716H, KBT 673F, KBW 341T na KBX 142P, ambazo zinaaminika kutumiwa kwa shughuli za wizi.
Okondo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Oruba, akitarajiwa kufikishwa mahakamani.