Muungano wa makundi ya waasi katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, umetangaza kusitishwa kwa vita kuanzia leo Jumanne.
Kwenye taarifa, muungano huo unaojumuisha kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda la M23, ulisema umeafikia hatua hiyo ili kuepusha maafa kwa raia.
Umoja wa Mataifa umesema watu wapatao 900 wameuawa na wengine 2,880 kujeruhiwa kwenye mapigano ya hivi punde kufutia kutwaliwa kwa mji wa Goma ambao ndio mji mkuu wa eneo la mashariki mwa DRC.
Muungano huo unaotambulika kama “Congo River Alliance” umeshutumu majeshi ya serikali ya DRC kwa kutekeleza mashambulizi ya angani dhidi ya raia katika sehemu zinazodhibitiwa na waasi.
Aidha, umesema hauna dhamira ya kutwaa udhibiti wa sehemu nyingine na kwamba umejitolea kulinda haki za raia.
Vita baina ya waasi na majeshi ya serikali vimesababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao katika muda wa miaka 3 iliyopita.
Kulingana na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, watu laki 4 wameachwa bila makao tangu mwezi Januari mwaka huu.