Bunge la Seneti litaandaa mkutano wa siku tatu kuanzia Jumatano hadi Ijumaa mjini Naivasha, kupanga mikakati ya vikao vya awamu ijayo ya nne itakayoanza Februari 11, 2025.
Maudhui ya mkutano huo ni “Kujenga sifa ya Bunge la Beneti, kupitia mikakati na jinsi ya kusonga mbele” na unatarajiwa kuwaleta pamoja Maseneta na wadau wengine kutathmini utendakazi wa bunge hilo katika vikao vitatu vilivyopita.
Spika wa bunge hilo Amason Kingi, atafungua rasmi mkutano huo ambao utawahusisha wawakilishi wa asasi za utawala na bunge ikiwa ni pamoja na serikali kuu, serikali za kaunti, Baraza la Magavana na Tume ya Ugavi wa Mapato.
Pia mkutano huo utatathmini ufanisi wa kamati za bunge hilo kwa kutambua mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo na kutafuta suluhu kwa changamoto hizo.
Aidha, Maseneta watajadili utekelezaji wa jukumu la Seneti la kusimamaia shughuli za serikali za magatuzi na pia kuangazia mapendekezo ya mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa kwa lengo la kubuni hazina ya shughuli za usimamizi wa kaunti kwa Maseneta.
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa anatarajiwa kuwataarifu Maseneta kuhusu hali halisi ya afya ya umma na kujadili mabadiliko yafaayo.