Serikali imezindua operesheni ya kiusalama kwa jina “Operation Ondoa Jangili” kwa lengo la kuwafurusha wahalifu katika kaunti za Marsabit na Isiolo.
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja anasema maeneo yanayolengwa katika operesheni hiyo ni pamoja na kaunti ndogo za Sololo, Moyale, North Horr na Merti yanayoshukiwa kuwa maficho ya kundli la waasi la Oromo Liberation Army (OLA) la nchini Ethiopia, kufanikisha uhalifu wa mipakani.
Operesheni hiyo inajiri baada ya machifu watano kudaiwa kutekwa nyara na washukiwa wa kundi la Al – Shabaab katika eneo la Elwak, kunti ya Mandera.
Kulingana na Kanja, operesheni hiyo inalenga kulinda maisha na mali na pia kudumisha amani katika eneo hilo.
“Kuambatana na jukumu la Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS) ya kulinda maisha na mali na kudumish amani, makundi maalum ya maafisa wa NPS yameanzisha awamu ya kwanza ya operesheni almaarufu ‘Operation Ondoa Jangili’ katika kaunti za Marsabit na Isiolo, kwa lengo la kuwafurusha wapigabaji wa OLA ambao wamejificha katika kaunti ndogo za Sololo, Moyale, North Horr, Merti,” alisema Kanja.
Wapiganaji wa OLA wamekashifiwa kwa kujihusisha na shughuli za uhalifu mipakani ikiwa ni pamoja na usafirishaji silaha haramu, mihadarati , ulanguzi wa binadamu, bidhaa haramu na uchimbaji haramu wa madini.