Rais Ruto awaondolea wafanyakazi wa zamani wa NHIF hofu ya kupoteza kazi

Martin Mwanje
1 Min Read

Hakuna mfanyakazi yeyote wa iliyokuwa Bima ya Kitaifa ya Afya, NHIF atakayepoteza kazi yake. 

Hakikisho hilo limetolewa na Rais William Ruto katika hotuba yake kwa taifa wakati wa sherehe za siku ya Mashujaa katika kaunti ya Kwale.

“Ninafahamu kuwa wakati wa kipindi hiki cha mpito, wafanyakazi wa iliyokuwa Bima ya Kitaifa ya Afya, NHIF watashughulikiwa kwa mujibu wa vifungu vya Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii ya mwaka 2023,” amesema Rais Ruto.

“Ninataka kuwahakikishia kuwa hakuna yeyote atakayepoteza kazi yake, na ninatambua kujitolea na huduma yao kwa taifa.”

Hakikisho hilo limekuja wakati moshi wa uvumi umekuwa ukifuka kwa muda kuwa wafanyakazi wa NHIF watapigwa kalamu baada ya kuanzishwa kwa bima mpya ya SHIF.

Ripoti ziliashiria kuwa hilo lingetokea kwa wafanyakazi hao kuhojiwa upya na wale ambao wangepatikana kuwa wanastahili kuendelea kuhudumu katika bima ya SHIF kuruhusiwa kufanya hivyo huku wasiostahili wakipigwa kalamu.

Ruto akitumia sherehe hizo za mashujaa kutoa wito kwa Wakenya kujiandikisha kwenye bima ya SHIF ambayo alisema hivi karibuni itafungua milango ya upatikanaji wa afya kwa wote nchini.

Hadi kufikia sasa, Rais amesema Wakenya milioni 12.9 wamejiandikisha kwenye bima hiyo.

Share This Article