Naibu Rais Rigathi Gachagua amemwelekezea kidole cha lawama Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, NIS Noordine Haji kwa kile alichokitaja kuwa utepetevu katika utendakazi wake.
Akizungumza Jumatano jioni kutoka kaunti ya Mombasa, Gachagua alisema kuwa NIS ilishindwa kumpa Rais taarifa za kiujasusi kuhusu waandamanaji waliovunja na kuingia ndani ya bunge.
Kulingana naye, ikiwa NIS ingefanya kazi yake ipasavyo, basi ingemtaarifu mapema Rais Ruto kwamba Wakenya wengi walipinga Mswada wa Fedha 2024 na hivyo kutoshinikiza mswada huo kupitishwa bungeni.
Kwa kufanya hivyo mapema, maafa yaliyoshuhudiwa Jumanne wiki hii hayangetokea.
Matamshi yake yanakuja wakati kumekuwa na madai kuwa tofauti zimechipuka kati yake na Rais William Ruto.
Wakati wa mkutano wake na wanahabari, Gachagua alionekana kulalamikia kutengwa katika ufanywaji wa maamuzi muhimu serikalini.