Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa viongozi wa upinzani anaosema wana nia ya kuupindua utawala wake akisema hawatafanikiwa katika njama yao.
Amesema yeyote mwenye nia ya kumbandua madarakani anapaswa kusubiri hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ili afanye hivyo kwa kufuata katiba.
Wakati huohuo, Ruto ameonya wale wanaochochea na kushiriki vurugu nchini akisema chuma chao ki motoni.
“Kama wako na mpango, tukutane 2027. Lakini njia ya mkato hapa katikati, hakuna. Nchi hii haitaharibiwa na watu wachache ambao hawana subira na wanataka kubadili serikali kutumia njia zisizokuwa za kikatiba,” alisema Rais Ruto leo Jumatano wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba 542 katika kituo cha polisi cha Kilimani katika eneo bunge la Dagoretti Kaskazini, jijini Nairobi.
“Wale wote ambao watapatikana katika njama ya kupora, kuchoma na kuharibu mali ya wananchi na biashara za watu wengine watachukuliwa hatua ya sheria. Na viongozi wao, tunawakujia. Huwezi ukachochea vurugu na kutarajia kukosa kuchukuliwa hatua.”
Wala Rais Ruto hakukomea hapo. Aliwataja kuwa magaidi watu wanaowashambulia Wakenya na maafisa wa usalama akisema kamwe utawala wake hautakubali hilo kutokea tena nchini.
“Wale wanaowashambulia Wakenya, maafisa wa polisi, vituo vya usalama na biashara ni magaidi. Vitendo kama hivyo vya kigaidi ni tangazo la vita. Hatutakubali nchi yetu kuharibiwa na watu wasiopenda maendeleo ambao wanatafuta njia ya mkato kuingia madarakani.”
Semi zake kali zinakuja wakati ambapo makumi ya Wakenya wamefariki kwenye maandamano ya Juni 25 na ya Saba Saba yaliyofanyika Julai 7 kulalamikia uongozi mbaya nchini.
Aidha, maafisa kadhaa wa polisi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo, vituo kadhaa vya polisi kuteketezwa na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa.
Tangu wakati huo, utawala wa Kenya Kwanza umeapa kuwachukulia hatua kali wale wote wanaochochea vurugu, na tayari wanasiasa kadhaa wamekamatwa kwa kuchochea vurugu hizo.