Mizozo katika chama cha ODM imeendelea kushamiri huku mbunge wa Gem Elisha Odhiambo akiwanyoshea Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna na Naibu kiongozi wa chama Arati Simba kwa kuchochea migawanyiko inayotishia kukisambaratisha chama.
Gavana wa Kisumu Prof. Anyang’ Nyong’o kwa sasa ni kaimu kiongozi wa chama hicho kufuatia hatua ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kuachilia wadhifa huo ili kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Sifuna amekuwa mstari wa mbele kuukosoa utawala wa Kenya Kwanza katika msimamo ambao umeungwa mkono na Arati ambaye pia ni Gavana wa Kisii.
Katika kumuunga mkono Sifuna, Arati anasema ODM si mwanachama wa serikali na kwamba anachokisema Sifuna ndio msimamo wa ODM kwani yeye ndiye Katibu Mkuu wa chama.
Akiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge leo Jumanne, Odhiambo ameonya kuwa mivutano inayoshuhudiwa chamani inaweza ikakisambaratisha.
“Wakati ambapo ODM inapaswa kuwa inaongeza ushawishi wake na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, viongozi hawa wawili wameazimia kuchochea usaliti, migawanyiko na kucheza na hatari kwa kutojali, yote hayo kwa kujitafutia umaarufu wa kisiasa,” alisema Odhiambo.
Hususan, Odhiambo alimshutumu Sifuna kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kama Katibu Mkuu.
“Badala ya kutoa uongozi wa kimkakati, Sifuna amekuwa sura ya mizozo ndani ya ODM, akikumbatia sarakatasi za kisiasa badala ya mazungumzo yenye tija.”
Chama cha ODM kimegawanyika katikati huku baadhi ya wanachama wakiunga mkono serkali ya Rais William Ruto na wengine wakiishutumu kwa madai ya kuwa chanzo cha mahangaiko wanayopitia Wakenya.
Baadhi ya wanachama wa ODM wameteuliwa serikalini kuwa Mawaziri.
John Mbadi anahudumu kama Waziri wa Fedha, Opiyo Wandayi kama Waziri wa Nishati, Hassan Joho kama Waziri wa Madini wakati Wycliffe Oparanya akihudumu kama Waziri wa Vyama vya Ushirika.
Uteuzi wa wanne hao umesababisha baadhi ya viongozi wa ODM kuwa wafuasi sugu wa serikali ya Kenya Kwanza na wale wanaoipinga serikali kusutwa vikali.