Muungano wa kiisilamu wa kijeshi kuhusu kukabiliana na ugaidi – IMCTC leo umezindua rasmi mpango wa mafunzo kuhusu kukabiliana na ufadhili wa ugaidi na utakatishaji wa fedha.
Hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika jiji kuu la Kenya Nairobi, ilihudhuriwa na waziri wa ulinzi wa Kenya Soipan Tuya na katibu mkuu wa IMCTC Meja Jenerali Mohammed bin Saeed Al-Moghedi.
Mafunzo hayo ambayo ni mojawapo ya mikakati ya IMCTC yamewaleta pamoja wawakilishi wa mashirika ya serikali, mamlaka za udhibiti, taasisi za kifedha na vyombo vya utekelezaji wa sheria.
Katika hotuba yake, Waziri Soipan Tuya alisema uzinduzi wa mpango huo wa mafunzo unathibitisha dhamira ya pamoja ya kuimarisha usalama wa kikanda na kimataifa.
Alisisitiza kwamba Kenya inatambua kikamilifu umuhimu wa juhudi madhubuti za kupambana na ufadhili wa ugaidi ambazo zinahitaji ushirikiano wa kimataifa ulio thabiti, kubadilishana taarifa, uratibu wa kisheria na maendeleo endelevu ya uwezo.
Waziri huyo aliongeza kusema kwamba ufadhili wa ugaidi unaendelea kuchochea usajili, upangaji, msaada wa vifaa na utekelezaji wa shughuli za kigaidi.
Alishauri kwamba bila kushughulikia vyanzo vya kifedha vinavyosaidia shughuli hizi, juhudi za kupambana na ugaidi zitaendelea kuwa hatarini.
Tuya alisifia ushirikiano wa Kenya na IMCTC, akibainisha kuwa Muungano huu unaunganisha nchi wanachama kwa lengo la pamoja la kupambana na misimamo mikali na vurugu kwa namna zote.
Katibu mkuu wa muungano wa kiisilamu wa kijeshi kuhusu kukabiliana na ugaidi – IMCTC Meja Jenerali Mohammed bin Saeed Al-Moghedi naye alihutubia mkutano huo wa uzinduzi.
Alisema kwamba tishio la ugaidi halina mipaka na halibagui kati ya mataifa, linalenga usalama, uthabiti na maendeleo kote duniani.
Bin Saeed Al-Moghedi alisisitiza kwamba Kenya ina jukumu muhimu katika kushughulikia changamoto na vitisho vya kiusalama barani Afrika.
Aliongeza kwamba, “Kuanzishwa kwa IMCTC kulijengwa juu ya dira wazi ya kuratibu juhudi za kimataifa na kuunganisha nguvu katika kuimarisha uwezo wa kiitikadi, kimtandao, kifedha na kijeshi.”
Katibu huyo alielezea kwamba mMkakati wa IMCTC unaruhusu utekelezaji wa mipango inayolenga kujenga uwezo na kutoa mafunzo kwa wataalamu ili kuongeza utayari wa taasisi zinazohusika na kupambana na ugaidi.
Aidha, alibainisha kuwa ufadhili wa ugaidi umekuwa uti wa mgongo wa makundi yenye misimamo mikali na ili kukabiliana nao ushirikiano ulioimarishwa unahitajika kati ya mataifa na taasisi za kifedha, pamoja na juhudi zilizoongezwa za kukabiliana na tishio hili.
Mpango huu unalenga kuanzisha uelewa wa kina kuhusu mifumo ya kisheria ya kimataifa, makubaliano yanayohusiana, uundaji wa zana za uchambuzi wa kifedha na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Mafunzo yatajumuisha mihadhara, warsha na vipindi vya mafunzo vinavyolenga mada kuu, ikiwa ni pamoja na mfumo wa kisheria wa kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, vyanzo na mbinu za uhalifu wa kifedha, mbinu za kugundua na kuchambua taarifa za kifedha, ushirikiano wa kikanda na kimataifa na mikakati ya kuzuia ufadhili wa ugaidi, utakatishaji fedha, mafunzo na uhamasishaji.