Rais Ruto atetea kuboreshwa kwa mpango wa Linda Mama

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametetea hatua ya serikali yake ya kuboresha mpango wa afya wa kina mama wajawazito na watoto wachanga Linda Mama, akisema idadi ya wanaonufaika iliongezeka.

Kiongozi wa nchi alisema kwamba mpango wa Linda Jamii, uliochukua mahala pa ule wa Linda Mama unatoa huduma jumuishi kwa familia nzima ikilinganishwa na Linda Mama uliokuwa ukinufaisha mama pekee.

Ruto alisema hayo leo katika chuo kikuu cha Umma katika kaunti ya Kajiado ambapo alizindua jengo la Dr Abdulrahman Al-Sumait lenye orofa 10, lililojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.4.

Rais aliwataka wakenya kumsamehe Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema kwamba mpango wa Linda mama ulitekeleza jukumu lake wakati wake na sasa umeboreshwa kwa lengo la kufaidi watu zaidi.

“Linda Mama ilikuwa nzuri; Linda Jamii ni bora na pana. Haingazii mama pekee bali inafaidi familia nzima” alisema Rais Ruto.

Matamshi ya Rais Ruto yanajiri siku chache tu baada ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuikosoa serikali ya sasa kwa kusitisha mipango muhimu iliyoanzishwa akiwa madarakani kama mpango huo wa Linda Mama.

Kenyatta alizungumza hayo Ijumaa iliyopita katika mkutano mkuu wa wanachama wa chama cha Jubilee ambapo aliondokea uongozi wa chama hicho.

Mpango huo wa  Linda Mama ulianzishwa Juni, 2013 na serikali na ulikuwa unatoa huduma za bure bila malipo kwa kina mama wajawazito na wanao wachanga katika hospitali zote za umma.

Linda jamii kwa upande mwingine ilianzishwa Juni 2025 chini ya halmashauri ya afya ya Jamii SHA na inatoa huduma za afya bila malipo kwa  kina mama, watoto wao  na waume zao na unashughulikia huduma msingi na hata kuu.

Website |  + posts
Share This Article