Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga ameizuru familia ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang aliyefia mikononi mwa maafisa wa polisi katika njia ya kutatanisha.
Maraga ambaye ametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, alitangaza hilo kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa X.
“Nikiwa njiani kutoka mazishi ya rafiki yangu na mzee wa kanisa marehemu Elias Ochola, nilitumia muda mfupi kuzuru familia ya marehemu Albert Ojwang, nyumbani kwao katika kaunti ya Homa Bay,” aliandika Maraga huku akichapisha picha za tukio hilo.
Hata hivyo alielezea kwamba hakupata wazazi wa mwendazake nyumbani lakini alikutana na kujadiliana na watu wa familia yake ambapo alipata fursa ya kuwasilisha rambirambi zake.
Katika chapisho lake Maraga alisema pia kwamba mauaji ya Albert yatasalia kuwa ukumbusho wa kazi ambayo sisi wote tunastahili kufanya ili kuhakikisha haki, ukweli na hadhi ya maisha ya kila mkenya.
“Ninarejelea wito wangu wa kujiuzulu, kuondolewa afisini, kutiwa mbaroni na hatimaye kushtakiwa kwa Inspekta Jenerali wa polisi, Naibu Inspekta Jenerali wa polisi mkuu wa kitengo cha upelelezi wa jinai na wahusika wote” aliandika Maraga.
Anasisitiza kwamba washikilizi wa nyadhifa alizotaja wanafaa kuwajibishwa kwa jukumu walilotekeleza katika mauaji ya mwalimu Albert Ojwang.