NCIC yalaani vurugu za Homa Bay, yatoa wito wa kuvumiliana

Katika siku za hivi karibuni, wahuni wameibuka kuwa kero katika maeneo mbalimbali nchini na serikali imetakiwa kuwatokomeza kabla ya maji kuzidi unga.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mwenyekiti wa NCIC Dkt. Kepha Omae alipokutana na wadau mbalimbali awali

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, NCIC imelaani vurugu zilizoshuhudiwa katika kaunti ya Homa Bay jana Jumapili. 

Vurugu hizo zilitokea pale wahuni waliposhambulia msafara wa vuguvugu la upinzani la Linda Mwananchi lililopanga kuandaa mikutano ya kisiasa katika eneo hilo.

Kiasi kwamba wahuni hao waliziba baadhi ya barabara za kuingia katika mji wa Homa Bay na kuwalazimu viongozi wa Linda Mwananchi, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, kutumia vichochoro.

“NCIC inalaani vurugu za kisiasa na vitendo vya vurugu vilivyoshuhudiwa katika kaunti ya Homa Bay leo (jana Jumapili). Huu ni mwenendo usiofaa na wa kutia wasiwasi unaokiuka Katiba ya Kenya 2010 na Sehemu ya 13 na 62 ya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa,” alisema mwenyekiti wa NCIC Dkt. Kepha Omae kwenye taarifa.

“Vitendo kama hivyo vinaibua mashaka ya usalama kuhusu kulinda uhuru wa kikatiba.”

Dkt. Omae akiashiria kuwa tume hiyo imeanza mchakato wa kuwataka wanasiasa wanaofadhili vurugu hizo kufika mbele yake na kuwajibishwa.

Wiki chache, NCIC ilitoa orodha ya majina ya wanasiasa iliyosema wanachunguzwa kwa madai ya kutoa semi za chuki.

Orodha hiyo iliwahusisha mawaziri wawili ambao ni Aden Duale wa Afya na Geoffrey Ruku wa Utumishi wa Umma.

Wahuni wameibuka kuwa kero katika maeneo mbalimbali ya nchi, mara nyingi wakidaiwa kutumiwa na wanasiasa kuvuruga mikutano ya wapinzani wao miezi michache kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Wachambuzi wa mambo wanasema hali hiyo huenda ikatishia usalama wa taifa ikiwa haitakomeshwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Share This Article