Nyong’o: Tusihusishe Ruwaza ya 2060 na uchaguzi mkuu ujao

Gavana huyo wa Kisumu amewahimiza Wakenya kujiunga na mjadala huo kwa nia ya kubuni mpango wa Kenya na mikakati ya kuafikia malengo yao kwa ufanisi wa pamoja.

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya wahimizwa kutoingiza siasa kwenye Ruwaza ya mwaka 2060.

Gavana wa kaunti ya Kisumu Prof. Anyang Nyong’o ametoa wito kwa Wakenya kutohusisha Ruwaza ya mwaka 2060 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza Jumatano jijini Nairobi wakati wa mdahalo wa kitaifa kuhusu ruwaza ya maendeleo ya mwaka 2060, Gavana huyo alisema malengo ya maendeleo ya muda mrefu hayapaswi kuzingatia siasa au mfumo wa uchaguzi uliopo.

“Mjadala huu sio kuhusu uchaguzi mkuu. Kile ambacho Wakenya wanapaswa  kujifunza kutoka kwa mataifa ambayo yamefanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi, ni kwamba malengo ya muda mrefu hayapaswi kuvurugwa na mfumo wa uchaguzi na uongozi wa kisiasa unaotokana na chaguzi hizo,” alisema Prof. Nyong’o.

Aliwahimiza Wakenya kujiunga na mjadala huo kwa nia ya kubuni mpango wa Kenya na mikakati ya kuafikia malengo yao kwa ufanisi wa pamoja.

“Tujipatie muda bora kuwa na mdahalo jumuishi miongoni mwa Wakenya kuhusiana na mustakabali wa taifa letu,’ aliongeza Gavana huyo.

Alipohutubia taifa mwezi jana, Rais William Ruto alihakikishia taifa kuwa mchakato huo utakuwa jumuishi, wenye uwazi na unaoongozwa na wananchi, kwa sababu ruwaza haiwezi kubuniwa na serikali pekee.

Share This Article