Nancy Onyango ateuliwa mwenyekiti wa jopokazi la kuchunguza deni la taifa

Tom Mathinji
2 Min Read
Nancy Onyango.

Rais William Ruto leo Ijumaa amebuni Jopokazi la kufanya uchunguzi wa deni la taifa, huku akimteua Nancy onyango kuwa mwenyekiti wake.

Jopokazi hilo lilibuniwa kupitia gazeti rasmi la serikali la Julai 5, 2024, muda mfupi baada ya rais kuhutubia taifa katika Ikulu ya Rais, ambapo alitangaza mikakati ya kupunguza matumizi ya serikali kufuatia kuondolewa kwa Mswada wa Fedha 2024.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Prof. Luis G. Franceschi ambaye atakuwa mwenyekiti wa jopokazi hilo, Rais wa chama cha mawakili nchini (LSK) Faith Odhiambo, mwenyekiti wa ICPAK Phillip Kaikai, Rais wa chama cha wahandisi nchini Shammah Kiteme, na mtaalam wa sera na uongozi Vincent Kimosop.

Jopokazi hilo linatarajiwa kuchunguza deni la taifa na kutoa ripoti yake baada ya miezi mitatu.

“Jopokazi hilo litahudumu kwa muda wa miezi mitatu kuanzia tarehe ya kuteuliwa au jinsi ilivyoratibiwa katika gazeti rasmi la serikali,” ilisema ilani hiyo.

Rais Ruto pia amewateua Abraham Rugo na Aaron Thegeya kuwa makatibu wenza wa jopokazi hilo, huku makao yake yakiwa katika hazina ya taifa na mipango ya taifa Jijini Nairobi.

Katika hotuba yake, Rais Ruto alisema kupitia ukaguzi huo, wakenya watafahamu hali ya deni la taifa, matumizi ya rasilimali za taifa, huku likitoa mwongozo wa usimamizi wa deni la taifa kwa njia bora zaidi.

Kiongozi huyo wa taifa alisema deni la taifa linazidi kuibua wasiwasi hapa nchini, na hivyo ipo haja kwa wananchi kufahamishwa kuhusu deni hilo na jinsi rasilimali za umma zilivyotumiwa.

Website |  + posts
Share This Article