Gavana wa kaunti ya Nairobi Jonhstone Sakaja ameahidi kuboresha miundombinu ya jiji hilo tayari kwa kipute cha kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2027.
Kipute hicho kitaandaliwa kwa pmaoja na mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania.
Sakaja alitoa ahadi hiyo jana Jumatano punde baada ya ombi la pamoja la mataifa hayo matatu kupata haki za maandalizi.
Gavana huyo alisema watashirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha matayarisho yanakamilika kwa wakati ufaao.
Uwanja wa Joe Kadenge, zamani ukijulikana kama City Stadium ni mojawapo wa viwanja vilivyo katika himaya ya kaunti na ambao kwa sasa unakarabatiwa kuwa wa kiwango cha kimatifa.
Kaunti ya Nairobi imepangaa kujenga angalau viwaja 10 ikiwemo Dandora na Woodley ili kusaidia makuzi ya vipaji.
Miundombinu mingine muhimu kwa dimba hilo la mwaka 2027 ni barabara, mikahawa, usafiri na usalama.
Kenya inapaswa kuwa na viwanja viwili vya kuchezea mechi hizo na angalau vingine viwili vya mazoezi.
Itakuwa mara ya kwanza kwa ukanda wa CECAFA kuandaa kombe la AFCON tangu mwaka 1976.