Mwanamume ahukumiwa miaka 100 gereza kwa wizi wa kimabavu

Kesi hiyo ilihusu wizi wa bunduki aina ya AK-47 kutoka kituo kimoja cha polisi, na kutumia bunduki hiyo kutekeleza uhalifu wa kimabavu katika kaunti hiyo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwanamume afungwa miaka 100 gerezani kwa wizi wa kimabavu.

Mwanamume mwenye umri wa miaka 26, amefungwa miaka 100 gerezani baada ya kupatikana na kosa la wizi wa kimabavu, kaunti ya Kirinyaga.

Kesi hiyo ilihusu wizi wa bunduki aina ya AK-47 kutoka kituo kimoja cha polisi, na kutumia bunduki hiyo kutekeleza uhalifu wa kimabavu katika kaunti hiyo.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa akiwa amejihami na bunduki aina ya AK47, alimuibia mhudumu wa kituo cha kuuza petroli simu ya thamani ya shilingi 2,200 na pesa taslimu 31,430.

Kwenye kikao katika mahakama ya hakimu ya Kerugoya, mlalamishi alimtambua mshtakiwa huyo, akitoa ushahidi kwamba alimwona kwenye kituo hicho cha petroli, kabla ya kuvunja dirisha na kumnyooshea bunduki.

Huku akihofia maisha yake, mlalamishi atoroka kuelekea kwenye shamba la kahawa lililo karibu.

Upande wa mashtaka pia ulitoa ushahidi kumhusisha mshtakiwa na bunduki hiyo iliyoibwa. Maafisa wa polisi walisema mshtakiwa huyo aliwaelekeza alikoficha bunduki hiyo, ikiwa na risasi 18..

Mchunguzi wa bunduki alithibitisha kuwa mabaki ya risasi yaliyopatikana katika eneo la mkasa, yalifyetuliwa kutoka kwa bunduki hiyo.

Mahakama ilibainisha kuwa upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha kesi hiyo, na kumhukumu mshtakiwa miaka 100 gerezani.

Awali kwenye kesi tofauti mshtakiwa huyo alikuwa amehukumiwa miaka 40 gerezani kwa kosa sawia na hilo katika kaunti hiyo ya Kirinyaga.

TAGGED:
Share This Article