Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania, Juan Mata, ametangaza kustaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 38.
Mata anahitimisha ukurasa wa taaluma yake akiwa na mataji kadhaa kwenye mkoba wake, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia, ubingwa wa Ulaya pamoja na mataji makubwa ya vilabu.
Aliichezea Uhispania mechi 41 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Pia alishiriki katika ushindi wa Uhispania wa mabao 4-0 dhidi ya Italia kwenye fainali ya Kombe la Yuro mwaka 2012, ambapo alifunga bao la nne.
Mata alianza taaluma yake ya soka kwenye kilabu cha Valencia kabla ya kujiunga na Chelsea mwaka 2011.
Mata alijiunga na Manchester United mwaka 2014, ambako alifunga mabao 51 katika mechi 285 na kusaidia kilabu hicho kutwaa mataji ya Ligi ya Yuropa, Kombe la FA na Kombe la Ligi.
Baada ya kuondoka Manchester United mwaka 2022, aliendelea na safari yake ya soka katika vilabu vya Galatasaray nchini Uturuki, Vissel Kobe nchini Japan, pamoja na Western Sydney Wanderers na Melbourne Victory nchini Australia.
Katika tangazo lake la kustaafu, Mata alisema ataendelea kujihusisha na soka, akisisitiza kuwa ingawa anaacha kucheza kitaaluma, hataacha kuwa mwanasoka.