Wanabiashara Nairobi wamtetea Sakaja

Wamewataka viongozi wa kisiasa kuweka kipaumbele katika ukuaji wa uchumi, ajira na utulivu wa biashara badala ya kuchochea migawanyiko ya kikabila.

Marion Bosire
2 Min Read

Wanabiashara jijini Nairobi wamemuunga mkono Gavana Johnson Sakaja, huku wakimkosoa kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, kutokana na matamshi waliyoyataja kuwa ya uchochezi na yenye kuleta migawanyiko ya kikabila.

Wafanyabiashara hao wamewataka viongozi wa kisiasa kuweka kipaumbele katika ukuaji wa uchumi, ajira na utulivu wa biashara badala ya kuchochea migawanyiko ya kikabila kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kauli yao imefuatia matamshi ya Gachagua mnamo Novemba 17 alipokuwa akizindua ofisi za chama cha DCP katika Kaunti ya Nairobi, eneo la Kasarani.

Wakati huo, alitangaza kuwa chama chake kinalenga kuutwaa uongozi wa Nairobi katika uchaguzi wa 2027 na kumtaja Sakaja kuwa kiongozi “aliyetumiwa na kutupwa.”

Mfanyabiashara John Njuguna alisema wafanyabiashara hawatakubali wanasiasa kugawa wakazi wa Nairobi kwa misingi ya kikabila, akibainisha kuwa Sakaja amekuwa na uhusiano mzuri na jamii mbalimbali, zikiwemo za Mlima Kenya.

Alitaja miradi ya maendeleo ya gavana huyo, kama ujenzi wa masoko, viwanja vya michezo na mipango ya ajira, kama ushahidi wa kujitolea kwa serikali yake kuhudumia wakazi.

“Biashara inahitaji utulivu, sio vita vya kikabila. Viongozi wanapopigana kwa misingi ya ukabila, mfanyabiashara mdogo wa Gikomba, Marikiti, Muthurwa na Kangundo ndiye anaumia,” Njuguna alisema.

Beatrice Wangeci, aliyenufaika na mpango wa Nairobi Green Army, pia alimtetea Sakaja, akisema mpango huo umewaunganisha vijana kutoka jamii mbalimbali kupitia fursa za ajira.

Alisema mpango huo umewawezesha mamia ya vijana kujipatia kipato kupitia shughuli za usafi, kupanda miti na unadhifishaji wa jiji.

Wafanyabiashara hao pia wamemtaka Gachagua kukoma kumlenga gavana huyo kisiasa na kumpa nafasi ya kuendelea kutoa huduma kwa wakazi.

Wamesisitiza kuwa Nairobi ni ya Wakenya wote, wakitaka viongozi kukumbatia uongozi jumuishi na kampeni zinazozingatia sera na masuala ya maendeleo, wakionya kuwa migawanyiko ya kisiasa inaweza kudhoofisha imani ya wawekezaji na maisha ya wananchi.

Share This Article