Waziri wa Afya Aden Duale amesema serikali imefanikiwa kuwafikia watu wote 135 waliotangamana na wagonjwa wa Ebola na hivyo kuzidi kiwango cha asilimia 85 cha ufuatiliaji kinachohitajika duniani.
Ameongeza kuwa hakuna kisa chochote cha ugonjwa huo kimeripotiwa nchini, ikiwa zimetimia siku 6 tangu mgonjwa wa mwisho aliporuhusiwa kuondoka hospitalini.
Ikiwa Kenya itatimiza siku 42 bila kuripoti kisa chochote cha ugonjwa wa Ebola, basi itatangazwa kama nchi isiyokuwa na ugonjwa huo ifikiapo Disemba 23 mwaka huu.
“Uangalizi, upimaji wa wasafiri na hatua zingine za kukabiliana na ugonjwa huo bado zimeimarishwa mno,” amebainisha Duale.
Aliyasema hayo alipofika mbele ya kamati kuu ya Seneti kuhusu sheria ndogo inayoongozwa na Seneta Mwenda Gataya wakati wa kikao kilichoandaliwa Bunge Towers leo Jumanne.
Duale aliielezea kamati hiyo kuwa wasafiri zaidi ya 800,000 wamepimwa katika maeneo 26 ya kuingia nchini huku maafisa wapatao 5,000 wa kupambana na ugonjwa huo wakikaa chonjo.
Wahudumu wa afya 4,900 waliopewa mafunzo, timu 349 za kuitikia haraka mbiu ya mganga iliapo na maabara tano za kufanya vipimo pia zinasaidia katika maandalizi.
Waziri ametoa wito wa utekelezaji endelevu wa sheria ili kuimarisha ulinzi wa afya ya umma na uratibu wa uitikiaji.