Ikulu ya Nairobi ilikuwa kitovu cha mikutano iliyowaleta pamoja Rais William Ruto na viongozi mbalimbali wakati mikakati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ikianza kushika kasi.
Rais Ruto akikutana na Spika Moses Wetang’ula, Magavana, wabunge na maafisa wa serikali kutoka eneo la Magharibi kabla ya ziara aliopanga kufanya eneo hilo baadaye wiki hii.
“Tunadilisha maisha na taswira ya Magharibi mwa Kenya kwa njia nyingi. Katika kilimo, mageuzi katika sekta ya sukari yamefufua viwanda vya umma vilivyokaribia kuanguka wakati mmoja,” alisema Rais Ruto baada ya kukutana na viongozi hao.
“Leo hii, wakulima wanazalisha zaidi na kupata mazao zaidi wakati wafanyakazi wakilipwa kila mwezi.”

Ruto aliongeza kuwa utawala wake unafanya uwekezaji zaidi kuliko wakati wowote ule katika kaunti za Busia, Kakamega, Vihiga na Bungoma.
Uwekezaji huo unajumuisha ujenzi wa barabara, nyumba za gharama nafuu, utoaji wa huduma za afya, viwanda na maeneo maalum ya uchakataji.
Baadaye, Rais Ruto alikutana na kinara wa chama cha ODM Dkt. Oburu Oginga kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa ushirikiano wa serikali jumuishi inayovileta pamoja vyama vya UDA na ODM na muungano wa Kenya Kwanza.
“Tulisisitiza umuhimu wa ushirikiano endelevu wa kisiasa, uwiano wa kitaifa, usawa na dhamira ya pamoja ya kutoa kipaumbele kwa maslahi ya kitaifa na ya Wakenya kuliko kitu kingine chochohote,” alisema Ruto.
“Ustawi wa Kenya wakati wote unapaswa kusalia kipaumbele chetu cha pamoja.”
