Viongozi wa upinzani waapa kumwasilisha mgombea mmoja wa urais

KBC Digital News
2 Min Read

Viongozi wa upinzani wameendeleza mikakati ya kumwondoa Rais william Ruto madarakani katika uchaguzi mkuu ujao, wakati huu wakipeleka windawinda zao za kura katika mjini Kitale.

Waliozuru mji huo leo Jumanne ni pamoja na kinara wa chama cha People’s Renaissance party, PM Caleb Amisi, mwenzake wa People’s Libertaion Party, PLP Martha Karua, pamoja na kinara wa United Green Movement (UGM), David Maraga.

Wakizungumza wakati wa sherehe za makaribisho ya viongozi hao nyumbani kwa Amisi, wamesisitiza kuwa upinzani umeazimia kuunganisha nguvu na kukubaliana kuwa na mgombea mmoja wa urais atakayenyamana na Rais Ruto.

Wameeleza kuwa kuwa na mgombea mmoja ni njia mojawapo ya kuimarisha upinzani na kuongeza uwezekano wa kuibuka na ushindi dhidi ya utawala wa sasa.

Aidha, wameikosoa serikali ya Rais ruto kwa kile walichodai kuwa ni kuzorota kwa utawala bora, ufisadi na utekaji nyara wa asasi za umma, wakisema serikali watakayoundia itaweka misingi mipya ya uongozi unaowajibika, kupambana na ufisadi na kulinda rasilimali za umma.

Wakizungumzia suala la uchaguzi, viongozi hao wamesisitiza kuwa hawatakubali matokeo ya uchaguzi ikiwa yataathiriwa na udanganyifu, wakiahidi kuweka mikakati madhubuti ya kulinda kura na kuhakikisha kila kura inahesabiwa na kuheshimiwa.

Wamewataka Wakenya kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 na kutumia haki yao ya kidemokrasia kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wa uongozi wa nchi.

Taarifa ya Joseph Mwanjala 

Share This Article