Nandy azindua picha rasmi ya jalada la albamu ijayo ya 911

Kwa mujibu wa Nandy, jina la albamu hiyo lina maana ya kipekee na ya kibinafsi kwake.

Marion Bosire
1 Min Read

Nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini Tanzania, Nandy, anayefahamika pia kwa jina la ‘The African Princess’, ametambulisha rasmi picha ya jalada la albamu yake mpya inayosubiriwa kwa hamu, iitwayo “911”.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, mwimbaji huyo aliyeshinda tuzo mbalimbali alichapisha picha hiyo ya jalada na kuthibitisha kuwa albamu hiyo itatoka rasmi duniani kote Novemba 27, 2026.

Kwa mujibu wa Nandy, jina la albamu hiyo lina maana ya kipekee na ya kibinafsi kwake.

Ingawa nambari 911 inafahamika kimataifa kama namba ya kupiga simu wakati wa dharura, kwa Nandy ina maana maalumu inayohusisha siku yake ya kuzaliwa, Septemba 11 (9/11), pamoja na siku ya kuzaliwa kwa mama yake, Novemba 11 (11/11).

Albamu hiyo inatarajiwa kuwa na zaidi ya nyimbo 10, ukiwemo wimbo wake mpya uliotoka hivi karibuni, “Oya”.

Mashabiki pia wanatarajia kusikia ushirikiano wa kimuziki na wasanii mbalimbali wa kimataifa kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Ghana, Jamaica na Uingereza.

Zikiwa zimesalia siku 10 kabla ya albamu hiyo kutoka rasmi, matarajio yanaendelea kuongezeka Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani, huku mashabiki wakisubiri kazi hiyo inayotarajiwa kuwa miongoni mwa albamu kubwa za muziki wa Afrika mwaka huu.

Share This Article