Diamond afutilia mbali ziara ya Australia

Hatua hiyo ilichochewa na mzozo mkubwa wa kifedha kati ya waandaaji wa hafla hizo.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki nyota wa Tanzania, Diamond Platnumz, amefuta matamasha yake yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu ya ziara ya “Retro” mjini Perth na Melbourne nchini Australia.

Hatua ya msanii huyo ilichochewa na mzozo mkubwa wa kifedha kati ya waandaaji wa hafla hizo.

Katika taarifa rasmi, kampuni inayomsimamia msanii huyo, Wasafi Limited, ilifichua kuwa promota mmoja wa nchini Australia anadaiwa kuzuia mapato ya mauzo ya tiketi, hali iliyowafanya waandaaji kushindwa kupata kumbi na huduma muhimu za maandalizi.

Matamasha hayo ya siku mbili yalikuwa tayari yamevutia mashabiki wengi, huku tiketi 4,452 zikiuzwa na kuingiza takriban dola 559,445 za Marekani, sawa na Shilingi milioni 72 za Kenya au Shilingi bilioni 1.5 za Tanzania.

Kufuatia kuvurugika kwa maandalizi, Diamond Platnumz alilazimika kurejea nyumbani licha ya kuwa tayari alikuwa amewasili nchini Australia kwa ajili ya maonyesho hayo.

Wasanii wengine waliokuwa wamepangwa kutumbuiza ni gwiji wa muziki wa dancehall kutoka Jamaica, Konshens, na msanii wa Afrika Kusini, Dlala Thukzin.

“Tunawaomba radhi kwa dhati maelfu ya mashabiki wetu waliokuwa wakisubiri matukio haya kwa hamu,” ilisema taarifa ya uongozi wa Wasafi, ikiongeza kuwa hatua za kisheria zinafuatiliwa dhidi ya wahusika.

Kampuni ya mauzo ya tiketi, We On Au, inatarajiwa kusimamia mchakato wa kurejesha fedha kwa mashabiki walioathirika.

Share This Article