Tanzania yaandikisha historia katika mashindano ya ulimbwende

Jihan Mohin Dimachk, wa Tanzania aliibuka mshindi katika mashindano ya ulimbwende ya Miss Grand International 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Taifa jirani la Tanzania limeandikisha historia katika mashindano ya ulimbwende ya Miss Grand International 2026 baada ya kuibuka mshindi na kuwa taifa la kwanza Afrika kuwahi kushinda.

Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano hayo, Jihan Mohin Dimachk, alitwaa taji la Miss Grand International 2026, na kuwa Mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushinda mashindano hayo ya kimataifa tangu yalipoanzishwa mwaka 2013.

Jihan aliweka historia hiyo jana Oktoba 10, 2026, katika fainali zilizofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand, akiiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee kwenye ramani ya mashindano ya urembo duniani.

Fainali hiyo iliwakutanisha washiriki 80 kutoka sehemu mbalimbali duniani ambapo Jihan alifanikiwa kutwaa taji lililokuwa likishikiliwa na Emma Mary Tiglao wa Ufilipino.

Mrembo Shyare Andrade kutoka Ecuador alimaliza katika nafasi ya pili, akifuatiwa na Beau Megan Goos kutoka Uholanzi, Ximena Carrillo kutoka Guatemala na Emoura Pham kutoka Vietnam.

Kwa mujibu wa wasifu wake kwenye tovuti rasmi ya Miss Grand International, Jihan ana asili ya Tanzania na Lebanon. Ameishi Tanzania, Lebanon na Msumbiji, huku uzoefu wake wa kikazi ukimfikisha pia nchini China, ambako amejihusisha na uanamitindo, mauzo na biashara kupitia majukwaa ya mtandaoni.

Share This Article