Akothee aibua maswali kuhusu mirahaba ya wasanii

Anadai kwamba yeye binafsi hajapokea mirahaba kutoka MCSK kwa miaka kadhaa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki na mfanyabiashara wa Kenya Akothee amezua maswali kuhusu usimamizi na usambazaji wa mirahaba ya wasanii.

Kupitia mitandao ya kijamii, msanii huyo amehimiza uwazi na uwajibikaji zaidi kutoka kwa shirika linalosimamia hakimiliki nchini, Music Copyright Society of Kenya, MCSK.

Katika chapisho lake Akothee, ambaye anajitambulisha kama msanii, mtaalamu wa rasilimali watu na mwanachama wa MCSK nambari 8592, alihoji ni kwa nini watumiaji wa muziki wanatakiwa kulipa ada za leseni huku baadhi ya wasanii wakisema hawajapokea mirahaba yao.

Alitoa mfano wa klabu ya burudani ya kaka yake iliyoko Mtwapa, ambayo alisema ilikuwa ikifuatiliwa kulipa ada ya kila mwaka ya leseni ya muziki ya shilingi 8,500.

Akothee alilinganisha hilo na madai yake kwamba yeye binafsi hajapokea mirahaba kutoka MCSK kwa miaka kadhaa.

“Ikiwa pesa zinakusanywa kote nchini kwa niaba ya wasanii, zinaenda wapi na zinasambazwa vipi?” aliuliza.

Mwanamuziki huyo pia alihoji kuhusu manufaa halisi yanayopatikana kwa wanachama wa MCSK, yakiwemo bima ya matibabu, mipango ya ustawi na usalama wa kifedha.

Akothee alisema anapanga kuzuru afisi za MCSK ili kupata ufafanuzi kuhusu masuala hayo akiwa mwanachama aliyesajiliwa.

Alitaka kukomeshwa kwa juhudi za mahusiano ya umma bila majibu ya kutosha, akisisitiza kuwa wasanii wanastahili uwazi na uwajibikaji kuhusu fedha zinazokusanywa kwa niaba yao.

Maswali hayo yanaibuka wakati mjadala kuhusu ukusanyaji na usambazaji wa mirahaba na ulinzi wa maslahi ya kifedha ya wasanii, unaendelea miongoni mwa wabunifu nchini Kenya.

Share This Article