Mwimbaji wa Kenya, Nadia Mukami, ametangaza ziara ya miji mitano nchini Marekani, ambako anatarajiwa kuwaburudisha mashabiki wake mwezi Novemba mwaka huu wa 2026.
Nadia alifichua ziara hiyo kupitia bango la matangazo lililochapishwa na Mizizi Group, likitangaza mfululizo wa maonyesho katika miji mbalimbali mikubwa nchini Marekani.
Ziara hiyo ya Nadia Mukami nchini Marekani itaanza Novemba 14 mjini Boston, kabla ya kuelekea Seattle Novemba 21.
Baada ya hapo, Nadia atatumbuiza huko Dallas Novemba 25, kabla ya kuelekea Minneapolis Novemba 27. Ziara hiyo itahitimishwa Novemba 28 katika eneo la DMV, linalojumuisha Washington, D.C., Maryland na Virginia.
Tangazo hilo limeongeza hamasa miongoni mwa mashabiki wa Nadia nchini Marekani, hasa Wakenya na wapenzi wa muziki wa Afrika wanaosubiri kumshuhudia msanii huyo akitumbuiza moja kwa moja.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za mwimbaji huyo kupanua ushawishi wake kimataifa na kuwasiliana zaidi na mashabiki wake wanaozidi kuongezeka nje ya Kenya.
Maelezo kuhusu maeneo ya maonyesho, tiketi na nafasi za kuhudhuria yanatarajiwa kutolewa na waandaaji. Mashabiki wanaotaka kupata taarifa zaidi wameelekezwa kuwasiliana na Mizizi Group kupitia mawasiliano yaliyo kwenye bango la ziara hiyo.
Haya yanajiri miezi michache tu baada ya onyesho lililofanikiwa la mwimbaji huyo nchini Kenya ambapo alikuwa anaadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki.