Filamu ya ‘Love in Every Word’ yarejeshwa YouTube

Kazi hiyo ya sanaa iliondolewa YouTube Jumanne Machi 11, 2025 kutokana na mzozo wa hakimiliki.

Marion Bosire
1 Min Read

Filamu iitwayo ‘Love in Every Word’ yake mwigizaji na mwandalizi wa filamu wa Nigeria Omoni Oboli imerejeshwa kwenye mtandao wa YouTube baada ya mzozo wa muda mfupi kuhusu hakimiliki.

Kazi hiyo ya sanaa ambayo ilikuwa imetizamwa zaidi ya mara milioni 5 katika muda wa siku tatu pekee, iliondolewa Jumanne Machi 11, 2025.

Chinonso Obiora maarufu kama Skyberry, ambaye ni mhandisi anayeishi nchini Canada na mmiliki wa studio za Skyberry zilizoko jijini Abuja nchini Nigeria ndiye alikuwa amewasilisha malalamishi ya hakimiliki.

Kuondolewa kwa filamu hiyo kulisababisha malalamiko kati ya wanamitandao wa Nigeria wanaompenda Oboli, lakini amejitokeza na kuelezea kilichotokea.

Kulingana naye, hatua hiyo ilitokana na kutokuelewana kati yake na Chinonso lakini kila kitu kimesuluhishwa ndiposa filamu hiyo imerejeshwa.

Mwigizaji huyo wa kike ambaye pia huishi nchini canada anashukuru mashabiki wake kwa kusimama naye wakati wa mtafaruku huo huku akiwahakikishia kwamba kila kitu kiko sawa.

“Tunashukuru sana kwa simu zenu jumbe, machapisho, maoni na kila kitu. Samahani singeweza kuwajibu nyote kwa wakati.” aliandika Oboli kwenye Instagram.

Hakuelezea zaidi kuhusu kilichotokea lakini alihimiza wanamitandao waendelee kuburudika na kazi hiyo ya sanaa huku akiwachapishia kuingo cha kuifikia.

Website |  + posts
Share This Article