Mwanamume mwenye umri wa miaka 65 amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumdhulumu kimapenzi mtoto mwenye umri wa miaka 11 katika kaunti ya Tana River.
Hakimu Mkuu Mwandamizi Edward Too alimpata mwanamume huyo na hatia ambayo aliitekeleza katika kijiji cha Kone tarehe tofauti mwezi Oktoba mwaka 2025.
Too alishikilia kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mshatikwa alitekeleza kosa hilo, akisema utetezi wa mshtakiwa huyo haukuwa na mashiko yoyote.
Mahakama ilidokeza kuwa ushahidi wa mtoto huyo haukubadilika na uliambatana na taarifa ya daktari, pamoja na mashahidi wengine.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita, wakiwemo mwathiriwa, mamake, nyanya yake, afisa wa watoto wa kaunti hiyo ndogo, afisa wa matibabu na afisa wa uchunguzi.
Aidha, hakimu huyo alisema dhuluma dhidi ya mtoto husababisha kifungo cha maisha gerezani chini ya sehemu ya 8(2) ya sheria za dhuuma za kingono.
Mahakama hiyo ilisema hukumu hiyo inalenga kuwakinga watoto dhidi ya dhuluma za kingono.