Mbunge wa Ol Kalou marehemu David Kiaraho kuzikwa Aprili 10

Tom Mathinji
1 Min Read
Marehemu mbunge wa Ol Kalou David Njuguna Kiaraho.

Kamati ya mipango ya mazishi ya marehemu mbunge wa Ol Kalou David Njuguna Kiaraho imetangaza kuwa mazishi yake yataandaliwa Ijumaa, Aprili 10, 2026 nyumbani kwake Tigoni, eneo bunge la Limuru.

Akitoa tangazo hilo, mwenyekiti wa kamati hiyo Kwenya Thuku ambaye ni mbunge wa Kinangop alisema mbunge huyo atazikwa kulingana mapenzi yake.

“Mwenzetu atazikwa katika shamba lake la Tigoni. Alizuru eneo hilo mara kwa mara kupumzika na alipendekeza kuzikwa hapo,” alisema Thuku.

Kulingana na kamati hiyo, kutakuwa na ibada ya kumkumbuka mbunge huyo katika uwanja wa michezo wa Ol Kalou Aprili 7, 2026, ili kutoa fursa kwa wakazi wa eneo bunge hilo kumuomboleza kiongozi wao.

Ibada ya mazishi itaandaliwa katika kanisa la PCEA St. Andrew Nairobi, Ijumaa April 10, 2026, kabla ya mazishi katika shamba la Tigoni.

Marehemu Kiaraho alikuwa akihudumu muhula wake wa tatu kama mbunge wa Ol Kalaou huku akichaguliwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.

Share This Article