Serikali ya kaunti ya Garissa, imezindua kampeni ya siku 10, inayolenga kuwachanga mifungo 600,000 katika kaunti ndogo za Dadaab na Fafi.
Katika kampeni hiyo, mbuzi, kondoo, ngamia na ng’ombe watachanjwa bila malipo dhidi ya ugonjwa wa Peste des Petits Ruminants (PPR) pamoja na ule wa miguu na midomo.
Akiwahutubia wanahabari baada ya kuzindua kampeni hiyo, waziri wa mifugo katika kaunti hiyo Milgo Dubow, alisema zoezi hilo linatoa fursa kwa kaunti hizo ndogo mbili kukabiliana na magonjwa hayo.
“Kuzuka kwa ugonjwa wa migufo, kunaweza sababisha hasara kubwa, ufugaji ni uti wa mgongo kwa wakazi wa kaunti hizo mbili ndogo, na ndio sababu tumeanzisha zoezi hilo,” alisema Dubow.
Kulingana na Dubow, utoaji huo wa chanjo, utasababisha mifugo kuwa na kinga imara dhidi ya magonjwa na hivyo kusababisha uzalishaji na mapato yaliyoimarika.
“Awamu ya kwanza italenga kambi za wakimbizi na jamii zilizokaribu, awamu ya pili ikilenga zaidi jamii za eneo hilo,’ aliongeza Dubow.
Alitoa wito kwa wamiliki wa mifugo, kuhakikisha mifugo wao wanachanjwa.