Johansen Oduor ambaye ni mwanapatholojia mkuu wa serikali nchini amefichua kilichosababisha kifo cha mwanariasha Kelvin Kiptum.
Baada ya upasuaji wa mwili wa marehemu Kiptum, Oduor ameelezea kwamba Kiptum alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyopata kwenye ajali huko Kaptagat kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Oduor aliyezungumza na wanahabari punde baada ya kukamilisha zoezi hilo alisema hali ni sawia kwa kocha wa Kiptum, Gervais Hakizimana ambaye pia aliangamia kwenye ajali hiyo.
Kando na majeraha kwenye kichwa Kiptum aliumia pia kwenye mbavu na uti wake wa mgongo pia uliathirika vibaya.
Oduor alisema kwamba yeye na kundi lake wamechukua sampuni kutoka kwa mwili wa Kiptum ili kutekeleza vipimo zaidi ili kufahamu iwapo kulikuwa na kitu mwilini mwake kilichomfanya ahusike kwenye ajali.
Mwili wa Kiptum unatarajiwa kuzikwa Ijumaa nyumbani kwake hafla ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais William Ruto. Mwili wa kocha wake umezikwa leo nchini Rwanda na waziri wa michezo Ababu Namwamba amehudhuria hafla hiyo.