Maseneta wapigwa marufuku kusafiri nje ya nchi

Martin Mwanje
1 Min Read

Maseneta na wafanyakazi wa Bunge la Seneti wamepigwa marufuku kusafiri nje ya nchi kwa kipindi cha yamkini wiki mbili zijazo. 

Spika Amason Kingi anasema hatua hiyo inatokana na shughuli nyingi zinazolizonga bunge hilo wiki ijayo.

“Kama mnavyofahamu, Seneti ina shughuli nyingi za kuzingatiwa siku zijazo. Kwa kuzingatia uzito wa shughuli hizi, ni muhimu kwamba tuwepo katika Bunge la Seneti,” amesema Spika Kingi katika barua aliyoiandika jana Jumanne.

“Kwa misingi hii, safari zote za nje ya nchi za Maseneta na wafanyakazi wa Bunge la Seneti kuanzia sasa zimepigwa marufuku. Pia nazielekeza kamati zote kusitisha shughuli zake nje ya Nairobi kuanzia leo (jana Jumanne) Oktoba 8, 2024 hadi Jumamosi, Oktoba 19, 2024.”

Barua hiyo inakuja wakati Bunge la Seneti limepangiwa kujadili hoja ya kufurushwa kwa Gavana wa Kericho Erick Mutai mapema wiki ijayo.

Bunge la Seneti pia litaandaa kikao cha Maseneta wote Oktoba 16 na 17 kuangazia hoja ya kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ilipitishwa na wabunge 281 katika Bunge la Taifa jana Jumanne.

Wabunge 44 waliipinga huku mmoja akikosa kupiga kura.

Share This Article