JSC yakashifu utumizi wa silaha kwenye majengo ya Mahakama

Tom Mathinji
1 Min Read
Tume ya Huduma za Mahakama.

Tume ya Huduma za Mahakama Nchini (JSC), imekashifu vikali utumizi wa bunduki kwenye mahakama ya Ruiru, kaunti ya Kiambu siku ya Ijumaa.

Hatua hiyo ya JSC imejiri baada vurugu kushuhudiwa nje ya Mahakama ya Ruiru wakati wa kukamatwa tena kwa kiongozi wa vijana wa DCP  kaunti ya Kiambu Peter Kinyanjui, almaarufu Kawanjiru, muda mfupi baada ya kuachiliwa kwa dhamana.

Wakati wa vurugu hizo, maafisa wa polisi walifyetua risasi kwenye majengo ya mahakama walipokuwa wakimtia nguvuni Kinyanjui.

Kupitia kwa taarifa, Katibu wa JSC Winfridah Mokaya, alisema ingawa tume hiyo inatambua na kuheshimu mamlaka ya kikatiba ya polisi kutekeleza sheria na kuwakamata washukiwa, ufyatuaji wa risasi katika mazingira ya mahakama haukuwa halali.

Alisema hatua hiyo inahatarisha maisha ya raia, na kuitaja kuwa ni dharau kwa mamlaka na hadhi ya Mahakama. Mokaya aliwataka wahusika wote kujiepusha na vitendo vinavyoondoa imani kwa taasisi zinazohusika na utoaji haki.

Kinyanjui anasemekana kuchunguzwa kuhusiana na ghasia zilizotokea wakati wa maandamano ya GenZ ya Juni 25.

Website |  + posts
Share This Article